Trump hatiani tuhuma za udhalilishaji

0
314

Baraza la Waamuzi huko Manhattan, New. York, Marekani limemkuta na hatia Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump katika shauri la kumdhalilisha kijinsia mwandishi mashuhuri wa zamani wa habari nchini humo E. Jean Carroll, tukio lililotokea miaka ya 1990.

Katika shauri hilo lililosikilizwa na Wajumbe tisa wa Baraza hilo, E. Jean Carroll mwenye umri wa miaka 79 alidai kudhalilishwa kijinsia na Trump kwenye chumba cha kubadilishia nguo katika duka la kifahari jijini New York.

Hata hivyo Trump hajakutwa na kosa la moja kwa moja la kumdhalilisha Carroll .

Kosa la moja kwa moja ambalo Trump amekutwa nalo ni kumdhalilisha mwandishi huyo wa habari wa zamani kwa kumuita muongo na tapeli.

Baraza hilo la Waamuzi limemtaka Trump kumlipa mwanamke huyo Dola Milioni tano za Kimarekani kutokana na usumbufu aliomsababishia.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais huyo wa zamani wa Marekani Donald Trump kukutwa na hatia katika shauri la udhalilishaji wa kijinsia.

Trump mwenyewe amekana kuhusika na udhalilishaji huo wa kijinsia na Mwanasheria wake Joseph Tacopina amesema watakata rufaa.