Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amesema jumla ya baa na kumbi za starehe 89 zimefungiwa, baada ya kubainika kupiga kelele na mitetemo iliyozidi viwango vinavyotakiwa.
Dkt. Gwamaka amesema baa na kumbi hizo za starehe zimebainika katika operesheni iliyofanyika ndani ya muda wa wiki moja katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma.
Ameeleza hayo wakati akitoa mrejesho wa operesheni iliyofanywa na NEMC kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini kwa lengo la kubaini baa na kumbi za starehe zinazopiga muziki kwa sauti ya juu ambayo ni kinyume cha sheria ya mazingira ya mwaka 2014.
“Tumebaini na kufunga baa na kumbi za starehe 19 za Kinondoni, 25 Ilala, Kigamboni 22 na Temeke 12, jijini Dodoma ni tano na Mwanza ni sita. Maeneo haya tulioyafunga ni sugu na haikuwa mara ya kwanza kuwaonya hawa tuliowafungia.” Amesema Dkt. Gwamaka
Ameongeza kuwa siku za nyuma waliishawaonya na kuwaadhibu kwa kuwapiga faini, lakini waliendelea kukaidi na kutaja miongoni mwa baa sugu kuwa ni Bodroom, Wavuvi Camp, Wherehouse, Avoco, Kitambaa Cheupe, Element, Chako ni Chako, Rainbow Gentlemen, Liquid na Soweto.