Mtoto wako amejaliwa kuwa na vipawa?. Ni swali ambalo wazazi wengi hufikiria mara nyingi.
Watoto wengi wenye vipawa wanaweza kujifunza na kuchakata taarifa kwa haraka zaidi kuliko watoto wa umri wao.
Hata hivyo wataalam wa ‘Neuroscience’ wanasema kwamba vipawa hivyo ni tofauti kwa kila mtoto.
Megan Cannella, Meneja wa masuala ya huduma za kifamilia kutoka taasisi ya Davidson ya nchini Marekani amesema, kuna namna nyingi ya kumtambua mtoto mwenye vipawa ama karama.
Amesema ni kawaida kwa watoto wenye vipawa kuhangaika na kazi rahisi kama vile kufunga kamba za viatu au kukumbuka kupiga mswaki.
Mtoto mwenye vipawa mwenye umri wa miaka 8 ambaye ni wa darasa na kwanza au la pili anaweza kuonyesha ujuzi wa kusoma kama mwanafunzi wa darasa la saba, na anakuwa na uwezo wa kufanya hesabu kama mwanafunzi wa darasa la tano.
Wanasayansi wa Neva pia wanaeleza kuwa watoto wenye vipawa hupata athari kali zaidi za kimhemko kutokana na mazingira yanayomzunguka.
Wametolea mfano, watoto hao wanaweza kuwa na wakati mgumu kufurahia kutazama maoneesho yaliyoambatana na matukio ya huzuni.
Watoto hao wanapata hisia za juu na wanaweza kufadhaika na kuvunjika moyo wanapohisi kama hali si sawa, hivyo hawafurahishwi na kutazama filamu za kusikitisha.
Watoto wenye vipawa mara nyingi pia huwa wadadisi kwa kiwango kikubwa, hasa kuhusu masuala ya maisha.
Wanaweza kuwa na wasiwasi zaidi kuhusu masuala kama vile kifo, umaskini, mabadiliko ya hali ya hewa na ukosefu wa haki kuliko watoto wengine.
Maswali yanaweza kuanzia “Ni nini hutokea tunapokufa?”,
“Kwa nini mambo mabaya hutokea duniani?”.
Kwa upande wa masomo darasani wanahitaji sana kazi za kusisimua akili zao mara kwa mara, hivyo ikiwa shule haina changamoto au haimchangamshi vya kutosha, wanaweza kupoteza ari ya kusoma na hata kuishia kufeli.
Ingawa wanaweza kufanya kazi nyingi kwa urahisi, mara nyingi wana ujuzi bora wa kufikiria na kumbukumbu bora hivyo hawaoni tatizo kujaribu lolote pale wanapokwama.
Wazazi wanashauriwa kuwachunguza vema watoto wao ili kupata ufahamu bora zaidi wa yeye ni nani, na kumuwezesha ili kufikia uwezo wake kamili.