Wakandarasi wa ndani wameaswa kuachana na vitendo vya rushwa wakati wa kuomba zabuni.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) Mhandisi Joseph Nyamhanga amesema hatua hiyo itasaidia kukuza uwezo wa wakandarasi hao na kuweza kushindana na wakandarasi wakubwa na kuaminiwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa.
Mhandisi Nyamhanga alikuwa akifunga mkutano wa tatu wa kikanda wa mashauriano na wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2023 ulioanadaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi.
Amesema utoaji wa rushwa ili kupata zabuni hufifisha uwezo wa wakandarasi, kwa kutekeleza miradi kwa hasara.
Akiwasilisha maazimio ya wakandarasi hao waliyokubaliana katika mkutano huo wa siku mbili, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarisi Mhandisi Rhoben Nkori,amesema, miongoni mwa makubaliano waliyoazimia ni wakandarasi kuomba kuongezewa kiwango cha malipo ya awali kutoka asilimia 15 hadi asilimia 50 na kuomba gharama ya malipo ya miradi ya upendeleo iongezwe wigo kutoka shilingi Bilioni 10 hadi shilingi Bilioni 30.
Mkutano huo umewakutanisha wadau wa sekta ya ujenzi kutoka mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Manyara, Singida na Dodoma.