Mende apata umaarufu Met Gala

0
362

Siku ya ugeni ndio mende walioko ndani ya nyumba yako nao hupita kujitambulisha kuwa nao wapo.

Mgeni huyu ambaye wengi huamini uwepo wake ni ishara ya uchafu, alionekana kwenye ‘Red Carpet’ ya mastaa matajiri na mashuhuri duniani wakati wa Met Gala 2023.

Mende huyo alionekana akitembea kwenye ngazi za jumba la Makumbusho ya Sanaa ya Metropolitan nchini Marekani usiku wa kuamkia leo Mei 02, 2023 kabla tu ya mwanamuziki Robyn Rihanna Fenty maarufu Rihanna na mwenza wake A$AP Rocky kuingia mahali hapo.

Mpiga picha Kevin Mazur, aliipata picha hiyo na kuiweka kwenye ukurasa wa Twitter wa Jarida la Variety.

The Met Gala au Met Ball ni tamasha la mavazi la kila mwaka na linafanyika kwa lengo la kuchangisha pesa kwa ajili ya Taasisi ya Mavazi ya Metropolitan Museum of Art iliyopo jijini New York.

Mwaka huu pesa zilizochangiwa ni kwa ajili ya kumuenzi mwanamitindo wa Kijerumani, marehemu “Karl Lagerfeld: Line of Beauty”.