Wizara ya Mifugo yaomba Bilioni 295.9

0
175

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeliomba bunge kupitisha kiasi cha shilingi Bilioni 295.9 kama Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ameliomba Bunge kuidhinisha Shilingi 112,046,777,000.00 kwa ajili ya Sekta ya Mifugo (Fungu 99) na Shilingi 183,874,156,000.00 kwa ajili ya Sekta ya Uvuvi (Fungu 64).

Akiwasilisha Bungeni jijini Dodoma bajeti ya wizara hiyo waziri
Ulega amesema, fedha hizo pamoja mambo mengine zitatumika katika uendelezaji wa sekta ya mifugo kwa kufufua Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO ) na uongezaji thamani ya mazao ya bahari kama mwani na samaki.

Ameongeza kuwa katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imepanga kuendelea kujenga uwezo wa wafugaji na kuwapatia mifugo ya kisasa ili waweze kufuga kisasa na kuongeza thamani katika shughuli zao za ufugaji.

Waziri Ulega amesema pia Serikali imepanga kuwawezesha vijana kupata elimu na kisha kuwapatia ng’ombe 10 kila mmoja kwa ajili ya kuanza kufuga na kuendeleza sekta hiyo na kutoa ajira kwa vijana.