Wakamatwa na mifuko 141 ya mbolea

0
173

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuingiza nchini mifuko 141 ya mbolea yenye ujazo wa kilo 50 kila mmoja, inayodaiwa kuingizwa kutoka nchi jirani kinyume na utaratibu.

Taarifa ya Jeshi la Polisi kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa, mbolea hiyo imekamatwa ikiwa kwenye gari aina ya fuso T 390 ACF na imekamatwa katika kata ya Rau manispaa ya Moshi kwenye nyumba ya mfanyabiashara mmoja.

Polisi walifanya upekuzi katika nyumba hiyo na kukuta aina mbalimbali za mbolea ikiwemo Urea Borabora mifuko 36, Yara mifuko 17 pamoja na mifuko mitupu ya mbolea za aina mbalimbali.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Mfanyabiashara huyo amekuwa akiingiza mbolea kutoka nchi jirani bila kufuata utaratibu na huenda inachakachuliwa kabla ya kuingia sokoni.

Polisi wamesema baada ya uchunguzi kukamilika, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.