Milioni 10 kila goli Simba na Yanga Afrika

0
314

Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza fedha za motisha kwa timu za Simba na Yanga kutoka shilingi milioni 5 hadi shilingi milioni 10 endapo timu hizo zitafuzu kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia anazitakia kila la kheri Simba na Yanga na amewataka wachezaji kujituma uwanjani na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha wanashinda michezo ya kukamilisha robo fainali ili wafanikiwe kuingia nusu fainali ambapo kila goli litakuwa shilingi milioni 10.

Simba inacheza mchezo wa marudiano leo dhidi ya Wydad Casablanca nchini Morocco wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano siku ya Jumapili dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Simba inacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 1-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 2-0 ilioupata ugenini huko nchini Nigeria.

Aidha, Msigwa amesema magoli yatakayolipiwa shilingi milioni 10 ni yale yatakayofungwa katika dakika 90 za mchezo au dakika 120 na sio magoli ya penati.