Maadili mema yaanzie kwenye familia

0
194

Katibu Mkuu wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Shekh Hassan Chizenga amewataka Watanzania kuwalea watoto wao katika maadili mema na kukemea kwa nguvu vitendo visivyofaa katika jamii.

Sheikh Chizenga amesema, jamii isikubali kuingizwa katika mtego wa kuunga mkono tamaduni zisizofaa kwa vigezo vya misaada, ili kulinda utamaduni na hadhi za Watanzania.

Akitoa mawaidha wakati wa Swala ya Eid iliyofanyika Kitaifa katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI BAKWATA Makao Makuu Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Sheikh Chizenga amesema, maadili mema yaanzie katika ngazi ya familia na hivyo jamii izingatie malezi ya watoto.

Ameongeza kuwa hivi sasa jamii imekuwa na mgawanyiko kuhusu vitendo visivyofaa badala ya kuungana na kuvitokomeza, kwani vinaangamiza Taifa.

Sheikh Chizenga amewataka Waumini wa dini ya Kiislamu kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu hata baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ili funga zao ziweze kuwa na maana.

Swala hiyo ya Eid Kitaifa pia imehudhuruwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.