Klabu ya soka ya Simba inarejea kambini hii leo jioni kujiwinda na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya mabingwa watetezi Wydad Casablaca ya Morocco.
Afisa habari wa Simba, Ahmed Ally amewaambia waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam kuwa baada ya kumalizika kwa mchezo wao wa mwisho wa juma dhidi ya Yanga wachezaji walipewa mapumziko ya siku moja na leo wanarejea kambini.
“Mechi yetu dhidi ya Wydad AC itakuwa ni Jumamosi Aprili 22, 2023 saa 10:00 jioni. Mnakumbuka mechi za makundi tulicheza saa 1 usiku lakini mechi hii tumepata saa 10 na hilo ni baada ya kuwaomba CAF sababu itakuwa sikukuu ili kila Mwanasimba aje uwanjani,” amesema Ally.
“Baada ya kumnyoa mtani jana wachezaji walipata muda wa kupumzika na leo wameingia kambini na saa 10 jioni wataanza mazoezi kwenye uwanja wetu wa Mo Simba Arena.”
“Kuhusu majeruhi, Kanoute anasumbuliwa na nyonga na leo atawasili kambini kukutana na madaktari kama atakuwa sawa ataanza mazoezi, hivyo hivyo kwa Aishi Manula atakutana na madaktari kuangalia hali yake.”
“Mechi yetu itakuwa na VAR maofisa wake watafika kesho. Wydad AC na wao watafika kesho saa 5 asubuhi wakiwa na msafara wa watu 50 na watakuja na ndege ya kukodi. Waamuzi na wao watafika nchini kesho,”Ahmed Ally.