Waziri Nape : Changamoto za TTCL ni za kihistoria

0
191

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema, changamoto nyingi za kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ni za kihistoria.

Ametolea mfano taarifa ya ukaguzi ya mwaka 2017/2018 iliyoonesha jumla ya shilingi Bilioni 91.43 kama madeni yasiyo na vielelezo, tatizo lilionekana kuanzia taarifa za hesabu za mwaka 2009 ikiwa ni miaka mingi kabla ya Serikali kurudishiwa umiliki wa Kampuni hiyo ya Simu Tanzania.

Waziri Nape ameyasema hayo jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 23 nchini, baina ya TTCL na Kampuni ya HUAWEI Tanzania.

Amesema hatua hiyo ina lengo la kuboresha utendaji kazi wa TTCL, ikiwa ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja toka mabadiliko hayo yafanyike kampuni limepiga hatua.

Aidha, Waziri Nape ametoa rai kwa TTCL kuhakikisha inafanyia kazi maelekezo ya Rais Samia kwa TTCL, ya kuangalia maeneo ya kupunguza gharama na kuwekeza kwenye maeneo ambayo itaweza kufanya vizuri zaidi na kuzalisha faida.