Dkt.Mwinyi akutana na Tume ya Kuboresha Haki Jinai

0
193

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinasubiri kwa hamu ripoti ya Tume ya Maboresho ya Mifumo ya Taasisi za Haki Jinai.

Amesema ripoti hiyo itatoa mwanga kwa Serikali zote mbili juu kuboresha mifumo na taasisi zinazohusika na Haki Jinai, ili haki ipatikane kwa ufanisi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar alipokutana na ujumbe kutoka
Tume ya Maboresho ya Mifumo ya Taasisi za Haki Jinai
uliofika Ikulu, Zanzibar kujitambulisha.

Amesema kuwepo kwa tume hiyo kunaonesha dhahiri marekebisho yatakayohitajika kufanywa juu ya mfumo mzima wa utoaji haki, ikiwemo marekebisho ya kimuundo ya taasisi hizo za kisheria, hali aliyosema itakaleta ufanisi kwenye utekelezaji wa masuala ya haki.

Rais Mwinyi amesema ni matarajio yake kuwa mambo mazuri yatafuata baada ya kukamilika kwa kazi iliyopewa Tume hiyo ya kusikiliza taasisi mbalimbali zikiwemo asasi binasi na za Serikali, viongozi wa Kitaifa, Wananchi na wadau wengine.

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema ana matarajio makubwa kupitia mapendekezo yatakayokuwamo ndani ya ripoti hiyo ambayo itawasilishwa kwa Rais Samia Suhulu Hassan.

Naye, Mwenyekiti wa Tume hiyo ya Maboresho ya Mifumo ya Taasisi za Haki Jinai Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Othman Chande amesema, wanatarajia kuwa na ziara ya kikazi ya siku nne katika visiwa vya Unguja na Pemba, ambapo watazungumza na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi zinazoshughulikia haki jinai kama Jeshi la Polisi, Chuo cha Mafunzo, Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Zanzibar, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa Zanzibar (ZAECA), Uhamiaji, Mahakama na Mkemea Mkuu wa Serikali.