Baada ya droo ya Shirikisho la Soka Afrika kuonesha kuwa Yanga SC kutoka Tanzania itakutana na Rivers United FC ya nchini Nigeria, mshambuliaji tegemeo wa Yanga, Fiston Mayele amesema alikuwa anatamani sana wapangwe na timu hiyo.
Mayele amesema mwaka 2021 wakati wanatolewa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hakupata nafasi ya kucheza, hivyo tamanio lao ilikuwa wapangwe nao tena ili walipize kisasi.
Kwa upande wa Afisa Habari wa Yanga amesema “tuliyemtaka kaja,” akimaanisha Rivers United, huku akisema kauli mbiu kuelekea mchezo huo ni “Kisasi ni Haki,” akimaanisha kuwa watalipiza kisasi.
Timu hizi zilipokutana Septemba 2021, Rivers United ilishinda michezo yote miwili kwa jumla ya magoli 2-0, na sasa Yanga wataanza kutafuta nafasi ya kulipa kisasi ugenini.
Rais wa Yanga Mhandisi Hersi Said amesema, wanatambua uzuri wa mpinzani wao, ambaye sasa yupo nafasi ya nne kwenye ligi ya Nigeria, lakini wanaamini kuwa kikosi chao ni bora na kina motisha, na watashinda na kuweka historia ya kutinga nusu fainali.
Mshindi wa robo fainali ya nne, ambayo ni kati ya Yanga na River United, atakutana na mshindi wa robo fainali ya kwanza kati ya Pyramids FC na Marumo Gallants FC.