Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote kuendelea kutunza mazingira na kuhifadhi vyanzo vya maji, ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa maji na viumbe hai kwa uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo mkoani Mtwara wakati akizindua rasmi mbio za Mwenge wa Uhuru ambazo zitahitimishwa Oktoba 14 mwaka huu mkoani Manyara.
Aidha ametoa rai kwa Wananchi wote kuimarisha usawa na kutokomeza ukatili wa kijinsia na unyanyapaa, kuimarisha lishe na kuzuia rushwa kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumzia ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa amesema, unazingatia umuhimu wa kuhifadhi mazingira na kutunza vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi wa Taifa.
Ameongeza kuwa ujumbe huo unalenga kuwaelimisha na kuwahamasisha Wananchi wote kushiriki kikamilifu katika harakati za kutunza vyanzo vya maji.
Baada ya kuwashwa, Mwenge wa Uhuru umekabidhiwa kwa vijana sita wakiongozwa na Abdallah Shaibu kutoka mkoa wa Kaskazini Pemba, ambao watakuwa na jukumu la kuukimbiza katika mikoa yote nchini.