Marekani na Tanzania kuingia mkakati mpya wa ushirikiano kiuchumi

0
164

Marekani imetangaza mkakati mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania kutokana na mwenendo mzuri katika utawala bora na usimamizi wa haki za binadamu ambavyo kwa pamoja vina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris amesema uongozi bora huleta utulivu na usalama, utabirikiaji wa sera na utawala wa sheria ambavyo wawekezaji na wafanyabiashara wengi huzingatia kabla ya kuweka mitaji yao.

“Kwa ushirikiano, ni lengo letu kuongeza uwekezaji wetu nchini Tanzania na kukuza ushirikiano wetu wa kiuchumi,” amesema Kamala ambapo ili kufanikisha hayo, ametangaza mikakati mipya ya ushirikiano.

Kwanza, Export-Import Bank ya Marekani itasaini hati ya makubaliano na Tanzania ambayo itawezesha upatikanaji wa hadi dola za Kimarekani milioni 500 kupitia usafirishaji nje (export) wa Marekani kwenda Tanzania katika maeneo ya usafirishaji, miundombinu, teknolojia ya kidijitali na nishati salama.

Pili, amesema Marekani inazindua ushirikiano mpya kupitia teknolojia ya 5G na usalama wa kimtandao.

Aidha, amesema kuwa kazi inaendelea nchini Tanzania kujenga kiwanda cha kwanza na cha aina yake barani Afrika cha kuchakata madini ambayo yanatumika kwenye betri za magari ya kielektroniki, mkakati ambao utawezesha dunia kupata betri zenye madini kutoka Tanzania ifikapo mwaka 2026.

“Kuna fursa nyingi za ukuaji hapa [Tanzania] hivyo utawala wetu unashirikiana na wadau wengine kuangalia fursa zaidi za madini hayo kwenye ukanda huu ili yachakatwe kwenye kiwanda hicho,” amesisitiza Kamala.