Kenya watakiwa kukaa meza ya mazungumzo

0
325

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki ametaka kufikiwa kwa makubaliano ya amani nchini Kenya na kuwashauri wadau wanaohusika na siasa kukaa katika meza ya mazungumzo.

Katika taarifa yake
Moussa ameelezea umuhimu wa mshikamano na kuungwa mkono kwa Serikali ya Kenya katika jitihada za kuwa na umoja wa kitaifa na amani nchini humo.

Amesema anasikitishwa na vurugu zilizotokea kufuatia maandamano yaliyoanza Jumatatu wiki iliyopita na kusababisha uharibifu wa mali na kuingilia shughuli za kiuchumi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Umoja na Upatanisho nchini Kenya (NCIC) Mchungaji Samuel Kobia amesema, masuala kama ya kupanda kwa gharama za maisha, umaskini na umiliki wa ardhi ni masuala yanayostahili kujadiliwa na si kutafutiwa ufumbuzi kwa kuharibu wa mali.

Ameshauri kusitishwa kwa maandamano yaliyoitishwa na Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga kwa kuwa yanavuruga amani na badala yake ametaka mazungumzo yatumike kumaliza tofauti baina ya Serikali na uongozi wa muungano huo.

Nalo Baraza la Viongozi wa dini nchini Kenya limesisitiza umuhimu wa amani, huku likimshauri Rais William Ruto na Odinga ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya kuwaelekeza wafuasi wao kutenda mambo mema ili kuliepusha Taifa hilo kuingia katika vurugu.

Hapo jana waandamanaji wanaomuunga mkono Kiongozi huyo wa Muungano wa Azimio la Umoja waliandamana katika maeneo mbalimbali nchini humo, maandamano ambayo hata hivyo hayakuwa na kibali cha polisi.