Rais Samia Atunukiwa Tuzo Maalum

0
167

Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa tuzo maalum kutokana na juhudi zake za kuimarisha uhuru wa habari na haki ya wananchi kupata taarifa za kweli na sahihi.

Tuzo hiyo imetolewa na Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini katika hafla ya ufunguzi wa kikao kazi cha Maafisa hao kinachofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amekabidhi tuzo hiyo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia.

Akiizungumzia tuzo hiyo, Waziri Nape ameeleza,

“Tunatambua kazi nzuri inayofanywa na Rais, tunatoa tuzo hii tukitambua mchango wake katika kuimarisha uwazi kwa mambo yanayofanywa na Serikali, tumeshuhudia fedha zinakopwa na kutangazwa hadharani zinakwenda kufanya nini, huu ni uwazi mkubwa kabisa.”

“Tunatoa tuzo hii ili kutambua mchango wake katika kuhakikisha Watanzania wanakuwa na wigo mpana wa kupata taarifa za kweli na sahihi,” ameongeza Waziri Nape.