Rais Samia aongeza tiketi 5,000 kuiona Stars

0
217

Rais Samia Suluhu Hassan ameongeza tiketi alizotoa kwa ajili ya mashabiki kufikia 7,000 kutoka 2,000 za awali.

Tiketi hizo zitakazotolewa kwa mashabiki ni sehemu ya hamasa ya Rais kuelekea mchezo wa marudiano kati ya Tanzania na Uganda utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Machi 28 mwaka huu.

Tiketi hizo ni sehemu ya tiketi 20,000 ambazo Serikali inatoa kwa mashabiki bure kuingia uwanjani kuishangilia timu ya Taifa.

Katika mchezo huo, na ijayo, Rais pia ameahidi kutoa TZS milioni 10 kwa kila goli ambalo Taifa Stars itafunga.

Stars inahitaji alama tatu, ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2023, ambazo zitafanyika nchini Ivory Coast Januari 2024.

Endapo itafuzu, Stars itakuwa imefikia hatua hiyo kwa mara ya tatu, ambapo mara ya mwisho ilifuzu mwaka 2019.