Profesa kuishi chini ya maji siku 100

0
306

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Taasisi ya Chuo Kikuu cha Florida Kusini nchini Marekani iliyochapishwa mwezi huu, Profesa Joseph Dituri (55) wa chuo hicho anatarajia kuishi chini ya maji kwa siku mia moja ili kuweka rekodi mpya duniani kwa mtu aliyekaa muda mrefu zaidi chini ya maji na mwenye mwili wenye uwezo wa kuhimili mazingira ya tofauti kulinganisha na binadamu wengine.

Hadi sasa rekodi iliyowekwa duniani ni ile ya binadamu aliyeishi chini ya maji kwa siku 73.

Ili kufuatilia kwa ukaribu zaidi jinsi mwili wa mwanadamu unavyokabiliana na hali ya mabadiliko na shinikizo kutoka kwenye kina kirefu cha maji, Joseph Dituri ataishi umbali wa futi 30 chini ya maji katika makazi ya mita za mraba 100 yaliyopo huko Key Largo Florida.

Taarifa zinaeleza kuwa Profesa huyo atasimamiwa na timu ya wataalamu ambayo itakuwa makini kutoa ripoti juu ya afya yake kwa kupiga mbizi mara kwa mara hadi kwenye makazi yake ili kurekodi mfululizo wa vipimo vya hali na mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika mwili wake.

Jaribio hili la kuishi kwa kipindi kirefu chini ya maji limekuja baada ya Dituri kutambulisha nadharia yake iliyotokana na matokeo ya utafiti wa kisayansi kuwa seli iliyokumbwa na mazingira ya ongezeko la shinikizo iliongezeka mara mbili zaidi ndani ya siku tano.

Hii inamaanisha ongezeko la shinikizo linaweza kumsaidia binadamu kurefusha maisha na kuzuia magonjwa yatokanayo na uzee.

Kwa mujibu wa profesa Dituri, anategemea mwili wake kubadilika na kuwa na uwezo wa kuishi muda mrefu.

Profesa Dituri alianza kulitumikia Jeshi la wanamaji akiwa na umri wa miaka 28 kwa cheo cha afisa mzamiaji na baada ya kustaafu kazi hiyo mwaka 2012 alijiunga na Chuo kikuu cha Florida Kusini (USF) ili kupata digrii ya juu ya udaktari ya mafunzo kuhusu majeraha ya ubongo.