Kirusi cha Marburg chaua 5 Kagera

0
174

Watu watano kati ya nane waliokuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kirusi cha Marburg wamefariki dunia mkoani Kagera, baada ya kuibuka mlipuko wa ugonjwa huo mkoani humo.

Kufuatia kirusi hicho, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amewataka Wananchi kuchukua tahadhari na kufika hospitalini wanapoona dalili ya kutokwa na damu sehemu mbalimbali, kutapika, kuharisha, homa na kuishiwa nguvu na kwamba ugonjwa huo hauna tiba maalum.

Aidha Waziri Ummy amewataka Watumishi wa afya nchi nzima kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo na kubainisha kuwa ugonjwa haujasambaa katika maeneo mengine.

Kati ya watu watano waliofariki dunia mkoani Kagera, wanne ni wa familia moja na mmoja ni Mtumishi wa afya.

Ugonjwa wa Kirusi cha Marburg kwa mara ya kwanza ulibainika nchini Ujerumani mwaka 1967 ambapo kwa Afrika umewahi kuibuka katika nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).