Adebayor atundika daluga baada ya miaka 21

0
366

Aliyewahi kuwa mshambuliaji wa Arsenal na Manchester City, Emmanuel Adebayor ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 39.

Raia huyo wa Togo amewahi pia kuzichezea Monaco, Real Madrid, Tottenham na Crystal Palace katika miaka 21 ya maisha yake ya soka yaliyoanzia katika klabu ya Metz.

“Shukrani kwa mashabiki wangu ambao wamekuwa nami siku zote. Ninajihisi mwenye furaha sana kwa ajili ya kila kitu, na nina matamanio kwenye kinachofuata,” amesema kupitia video kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Katika maisha yake ya soka ametunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa Togo mara tano mfululizo kati ya mwaka 2005 na 2009.

Katika muongo mmoja aliocheza Ligi Kuu ya England akivaa uzi wa Spurs, Arsenal na Man City alifunga magoli 79.

Adebayor, moja ya majina makubwa ya Soka Afrika amestaafu akichezea klabu ya AC Semassi ya Togo.