Tanzania yafungua ubalozi Windhoek

0
153

Tanzania imefungua rasmi ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Windhoek nchini Namibia.

Hafla ya kufungua ofisi hizo imeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Tax na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania pamoja na Namibia.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Dkt. Tax ameishukuru Serikali ya Namibia hasa wizara ya Mambo ya Nje kwa ushirikiano ilioutoa katika hatua zote za kuanzisha ofisi hiyo pamoja na kushiriki tukio la kihistoria la ufunguzi ambalo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.

Amesema kutokana na Tanzania kuwa Mama wa Lugha ya Kiswahili, inaendelea na jitihada za makusudi za kuhakikisha lugha hiyo inatangazwa na kuenea kwa kasi kupitia Balozi zake, vyuo vya Kimataifa na majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

“Wakati huu ambapo Serikali za Tanzania na Namibia zipo kwenye mazungumzo ya lugha ya Kiswahili kuwa sehemu ya lugha ya chaguo katika shule za Namibia, Ubalozi umefungua maktaba ndogo yenye vitabu na majarida ya Kiswahili kwa ajili ya watu wenye nia ya kujifunza Kiswahili kuja kujisomea” amesema Dkt. Tax