CHADEMA wafunga maswali ya dodoso

0
142

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefunga kuwahoji wabunge watatu miongoni mwa 19 wa viti maalum waliofukuzwa uanachama wa chama hicho.

Akizungumza wakati kesi hiyo ilipoitwa leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Cyprian Mkahe kwa ajili ya Jesca Kishoa kuendelea kuhojiwa maswali ya dodoso, Wakili wa wajibu maombi Hekima Mwasipu amesema, kesi hiyo ilipaswa kuendelea kwa Mbunge Kishoa kuhojiwa, lakini kwa upande wao wamefunga suala hilo.

Wakili Mwasipu ameeleza kuwa baada ya kutafakari kwa kina na kushauriana na bodi ya wadhani ya CHADEMA, wameona wasiwe na maswali ya dodoso tena kwa waleta maombi Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.

Kwa upande wake Wakili wa waleta maombi Ipilinga Panya ameieleza mahakama hiyo kuwa hawana pingamizi na hoja zilizotolewa na wajibu maombi juu ya kufunga maswali ya dodoso kwa wateja wao.

Wabunge hao 19 wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee walifukuzwa uanachama mwezi Novemba mwaka 2020 baada ya kwenda bungeni Dodoma kuapishwa bila idhini ya chama hicho.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea kwa hatua ya mahojiano Machi 9 na 10 ambapo mawakili wa waleta maombi ambao ni Halima Mdee na wenzake wameomba baadhi ya wajumbe wa bodi ya wadhamini ya CHADEMA kufika mahakamani kwa ajili ya kuhojiwa.