Fei Toto vs Yanga muda wowote kuanzia sasa

0
896

Mwanasheria Fatma Karume ambaye anamwakilisha mchezaji Feisal Salum (Fei Toto) amesema kuwa wameiachia kamati itafakari upya maamuzi kuhusu mvutano wa kimkataba uliopo kati ya mchezaji huyo na Yanga SC.

Karume amesema hayo mara baada ya kutoka kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) jijini Dar es Salaam ambapo leo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo ilikuwa ikifanya mapitio, na kusema kikubwa watu wawe na subira.

Akijibu swali la mwandishi endapo anatamani kumwona Fei Toto akirejea uwanjani akiwa na Yanga amesema “kijana ana haki yeye kusema anataka kurudi au harudi.”

Kwa upande wa Yanga kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji, Andre Mtine imesema haina shaka na kwamba inasubiri jibu la mwisho la kamati.

“Tuliitwa kwenye review na tumekuja, tumesikilizwa na kusikiliza na sasa tunasubiri jibu la kamati tu,” amesema Mtine.

Kamati imesisitiza kuwa muda wowote baada ya kumalizika kwa kikao hicho itatoa majibu kamili.

Upande wa Fei Toto uliomba mapitio ya uamuzi wa TFF, kutokana na kutorodhika na uamuzi uliotolewa Januari 6 mwaka huu ambao ulieleza kuwa yeye ni mchezaji halali wa Yanga.