Baadhi ya akina Mama wanaojifungulia katika kituo cha afya cha Masumbwe kilichopo wilayani Mbongwe mkoani Geita, wameishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya katika kituo hicho ambapo kwa sasa wanapata dawa za kutosha tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Akina Mama hao wametoa shukrani hizo walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari wa TBC mkoani Geita wakati Mbunge wa Viti Maalum mkoani humo Rose Busiga alipofika kwenye kituo hicho cha Afya kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafuta ya kupaka, kanga na sabuni.
Wametoa rai kwa wadau wengine kuwasaidia kuwapatia vifaa mbalimbali kama alivyofanya Mbunge huyo, sababu wanapokuwa katika hali ya ujauzito na kujifungua wanahitaji msaada.
Kwa upande wake Mbunge huyo wa Viti Maalum wa mkoa wa Geita, Rose Busiga ameishukuru Serikali kwa kuwapatia dawa za kutosha katika kituo hicho cha Afya cha Masumbwe.
Matroni wa kituo hicho cha Afya Pascazia Amos amesema, kwa sasa dawa zinapatikana kwa asilimia 99 katika hicho ambacho wastani wa wanawake 12 wamekuwa wanajifungua ndani ya saa 24.