Mvua kubwa yaleta maafa Geita

0
216

Mtoto Marysiana Lucas (5) mkazi wa kijiji cha Bugogo halmashauri ya wilaya ya Geita amefariki dunia baada ya kudondokewa na ukuta alipokuwa akijitahidi kujiokoa baada ya mvua kubwa ya mawe kunyesha katika eneo hilo.

Watoto wengine wawili wamejeruhiwa katika tukio hilo ambapo mvua hiyo kubwa ya mawe iliambatana na upepo mkali.

Habari zaidi kutoka wilayani Geita zinaeleza kuwa nyumba 117 zimeezuliwa paa katika vijiji vya Bugogo, Ikina na Mtono kufuatia mvua hiyo kubwa iliyoambatana na upepo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani Geita, Cornel Magembe ametembelea vijiji hivyo na kukabidhi vyakula mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchele kilo 500, maharage kilo100 na mafuta ya kupikia lita 100 kwa watu waliothirika katika tukio hilo, vyakula vilivyotolewa na

mgodi wa dhahabu wa Buckreef.

Pia amekabidhi kilo 260 za mahindi zilizotolewa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita, Charles Kazungu.

Kamati iliyoundwa kuangalia athari zilizotokana na tukio hilo inaendelea kufanya tathmini na inatarajiwa kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha siku mbili.