Mwana FA ateuliwa Naibu Waziri

0
146

Rais Samia Suluhu Hassan amemteua Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA kuwa Naibu waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo kuchukua nafasi ya Pauline Gekul ambaye amehamishiwa wizara ya Katiba na Sheria.

Rais Pia ametengua uteuzi wa waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki na nafasi yake imechukuliwa na aliyekuwa Naibu waziri wa wizara hiyo Abdallah Ulega.

Katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri Rais pia amewahamisha wizara Manaibu Waziri watano ambapo David Silinde amehamishiwa wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Pauline Gekul amehamishiwa wizara ya Katiba na Sheria kuchukua nafasi ya Godfrey Pinda ambaye amehamishiwa wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa Naibu Waziri.

Rais amemhamisha wizara Deogratius Ndejembi kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alikokuwa Naibu waziri, kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Uapisho wa viongozi hao utafanyika saa 10 jioni, Jumatatu Februari 27, 2023 Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.