Bilioni 56 kutumika kuboresha mazingira ya biashara nchini

0
243

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema dira ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha mazingira ya sekta ya biashara na uwekezaji nchini pamoja na ushindani wa kibiashara ili kuiwezesha sekta hiyo kuchangamka na kuchangia kwa kasi kubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.

Ameyasema hayo alipokuwa akihitimisha Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya lililofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Rais Mwinyi amesema Serikali inathamini sana ushirikiano kutoka nchi za jumuiya ya Umoja wa Ulaya na kuishukuri jumuiya hiyo kwa kuipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 23 sawa na bilioni 56.98 ambazo zinakwenda kutekeleza programu ya uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na biashara inayojulikana kwa jina la BLUEPRINT, na pia itaboresha kazi ya udhibiti wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, Dkt. Mwinyi amesema kuwa TBS itahakikisha kwamba bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya ubora wa kimataifa, na hivyo kurahisisha ufikiaji wa masoko ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya.