Magari ya kubeba wanafunzi yagongana

0
2659

Mtu mmoja amekufa na wengine Kumi wamejeruhiwa wakiwemo wanafunzi Wanane baada ya magari mawili yaliyobeba wanafunzi wa shule za msingi Kivulini na Nyamuge kugongana uso kwa uso katika barabara kuu ya Mwanza – Simiyu eneo la Nyamhongolo jijini Mwanza.

Jeshi la polisi mkoani Mwanza limethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa imesababishwa na uzembe wa dereva wa gari la shule ya msingi Kivulini, – Kulwa Charles ambaye alihama upande wake na kwenda kuligonga gari la shule ya msingi Nyamuge lililokua kikiendeshwa na Albert Joram ambaye amefariki dunia.

Majeruhi wanane wa ajali hiyo wameruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu katika kituo cha afya cha Buzuluga na katika hospitali ya Sekou-Toure .

Majeruhi wawili ambao ni mwanafunzi Devotha Beni na dereva wa gari la shule ya msingi Kivulini, – Kulwa wamehamishiwa kwenye hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.