Mhandisi mstaafu wa umeme wa nchini Marekani, Bruce Campell (64) amegeuza ndege aina ya Boeing 727 kuwa nyumba ya makazi katikati ya msitu anapoishi kwa miaka zaidi ya 20.
Campell alinunua kiwanja cha ekari 10 kwa dola elfu 23 za Kimarekani kwenye msitu wa Hillsboro, Oregon.
Alipanga kujenga nyumba ya kisasa ya makazi katika eneo hilo, lakini alipata fununu kuwa yupo Mama Joanne Ussery anayeishi kwenye ndege.
Mhandisi huyo mstaafu alimtembelea Joanne na ndipo alipobadili mawazo ya kujenga nyumba.
Mwaka 1999, Campbell alinunua ndege aina ya Boeing 727 kutoka Olympic Airways kwa dola laki moja za Kimarekani .
Baada ya kuinunua alihitaji kuisafirisha hadi msituni na kwa kuwa ndege ilikuwa ikitokea Athens, Ugiriki, usafiri huo uligeuka kuwa wa gharama sana.
Gharama za usafiri ziliongezeka kwa dola 120,000 za Kimarekani hadi kuifikisha ndege hiyo katika eneo ambapo ndipo yalipo makazi yake kwa sasa.
Na hiyo ni kesema alitumia dola laki mbili na ishirini na kama ingekuwa ni pesa ya Tanzania Mhandisi huyo mstaafu wa umeme angekuwa ametumia shilingi milioni 512.2 kama gharama za kununua na kusafirisha ndege hiyo ambayo ni makazi yake ya sasa kwenye eneo hilo.
Hata hivyo Campbell anakiri kutojutia pesa hiyo, kwani alichokihitaji amekipata.