Madhara zaidi ya Ida yabainika Zimbabwe

0
367

Shughuli za uokoaji zinaendelea nchini Zimbabwe baada ya Kimbunga Ida kuyakumba maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kusababisha vifo vya watu kadhaa na uharibifu wa mali.

Habari kutoka nchini Zimbabwe zinasema kuwa watu 65 wamekufa kutokana na kimbunga hicho katika eneo la Mashariki pekee  la nchi hiyo, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka, kwa kuwa watu wengi hawajulikani walipo.

Miongoni mwa majimbo yaliyoathiriwa zaidi na kimbunga hicho ni jimbo la Manicaland lililopo karibu na eneo la mpaka wa Zimbabwe na Msumbiji, ambapo miundombinu yake mbalimbali imeharibika kabisa na hivyo kuleta adha kubwa kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.

Kufuatia kimbunga hicho ambacho kilikua kikisafiri umbali wa kilomita 177 kwa saa, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe ambaye alikua  ziarani Mashariki ya Kati, amelazimika kukatisha ziara yake na kurejea nchini humo.

Kimbunga hicho Ida pia kimeyakumba maeneo mbalimbali ya nchi za Msumbiji na Malawi  na kusababisha vifo vya takribani watu 120.