Monesho ya mitindo ya mavazi yanayowashirikisha wazee kama wanamitindo ni nadra sana kufanyika, tena lile litakalohusisha wanamitindo wazee wa Kiafrika ndio adimu zaidi kutokea.
Nchini Nigeria mtaalamu wa picha Malik Afegbua amepata umaarufu mkubwa duniani kote baada ya kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii mwezi Januari mwaka huu zikiwaonesha wazee katika mitindo ya mavazi wakiwa kwenye eneo la kuoneshea mavazi huku wakiwa wamevalia nguo maridadi za mitindo na zenye rangi za kuvutia.
Hata hivyo ukweli ni kwamba picha hizo za onesho la mitindo ya mavazi ya kisasa katika uhalisia halijawahi kutokea, ingawa picha zinaonekana kama ni picha za tukio la kweli zilizofanikishwa kwa njia ya akili bandia [artificial intelligence].
Ili kufanikisha onesho hilo, Malik alitumia jukwaa la akili bandia liitwalo Midjourney linalotengeneza picha za maonesho zikiambatana na maandishi.
Onesho hilo lilikusudiwa kuipinga dhana potofu kuhusu namna watu wenye umri mkubwa wanavyotafsiriwa katika ulimwengu wa mitindo ya mavazi wakiwekwa nyuma katika masuala ya mitindo.