Serikali yabaini upotevu wa dawa Babati

0
226

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amebaini mianya ya upotevu wa dawa katika hospitali ya wilaya ya Babati mkoani Manyara na kutoa muda wa siku saba timu maalum kufanya uchunguzi wa mfumo wa uagizaji, utunzaji na utoaji wa dawa katika hospitali hiyo.

Dkt. Dugange amebaini upotevu huo wakati akikagua utoaji huduma katika hospitali ya wilaya ya Babati, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani Manyara.

“Sijaridhishwa na utunzaji wa takwimu za uagizaji, utunzaji na utoaji wa dawa kwa wagonjwa, vilevile dawa hazipatika kwa kiwango kinachotakiwa katika Bohari ya Dawa katika hospitali hii.” amesema Dkt. Dugange

Amesema serikali imeweka utaratibu wa kuagiza dawa, kupokea, kutunza na kutoa dawa kwa wagonjwa lakini taratibu hizo hazifuatwi jambo ambalo linatoa mianya ya wizi wa dawa katika hospitali hiyo ya wilaya ya Babati.

Dkt. Dugange amemuagiza Katibu Tawala wa mkoa Manyara ndani ya siku saba ahakikishe anapeleka timu maalum ya kufanya uchunguzi wa uingazaji, utunzaji na utoaji wa dawa ili hatua stahiki zichukuliwe endapo kutabainika kuwepo kwa upotevu.

Pia amebaini uzembe katika usimamizi wa ujenzi wa wodi tatu na jengo la kuhifadhi maiti katika hospitali hiyo ambapo serikali ilipeleka shilingi milioni 750 lakini fedha hizo zipo kwenye akaunti kwa zaidi ya miezi mitatu na hakuna kazi iliyofanyika.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI ameagiza ifikapo tarehe 30 mwezi Mei mwaka huu ujenzi huo uwe umekamilika.