Mbaroni wakituhumiwa kumshambulia mwanafunzi

0
153

Jeshi la polisi mkoani Mbeya linamshikilia Mwalimu wa shule ya sekondari Loileri iliyopo mji mdogo wa Mbalizi mkoani humo Peter Emmanuel (29) pamoja na mlinzi wa shule hiyo Haruna Issa (30) mkazi wa Iwala, kwa tuhuma za kumshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili mwanafunzi kidato cha nne wa shule hiyo Laurance Nicholous.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwanafunzi huyo kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu.

Amesema mwalimu na mlinzi huyo walimshambulia Laurance wakimtuhumu kuiba maandazi katika duka la shule hiyo.

Mwanafunzi huyo amepata majeraha sehemu ya paji la uso, mkono wa kushoto na kwenye magoti yote mawili.

Kamanda Kuzaga amesema, baada ya kumshambulia na kumjeruhi mwanafunzi huyo, mwalimu huyo pamoja na mlinzi walimpeleka hospitali teule ya Ifisi ili akapatiwe matibabu.

Amesema upelelezi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.