Simba: Rais Samia ametuongezea hamasa

0
185

Simba SC kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii imeeleza kupokea kwa furaha hamasa iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa atatoa TZS milioni 5 kwa kila goli ambalo timu hiyo pamoja na Yanga zitafunga katika michezo ya kimataifa mwisho wa wiki.

“[Shilingi] milioni 5 kwa kila goli. Tunakushukuru jemedari wetu, Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea hamasa. Vijana wako imara na hamasa yako imekuja muda muafaka,” imesema Simba.

Aidha, imeeleza kuwa “tunatambua mchango mkubwa wa serikali kwenye kuendeleza michezo, na ndio maana tuliamua kuiweka nchi mbele kwa kutangaza vivutio vyetu vya utalii.”

Rais Samia kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii baada ya taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali amezitakia timu hizo heri katika michezo yao.

“Michuano ya CAF mwaka huu tunawakilishwa na watani wa jadi, Simba (Klabu Bingwa) na Yanga (Kombe la Shirikisho). Kama alivyowajulisha Msemaji Mkuu wa Serikali, natoa hamasa ya Shilingi Milioni 5 kwa timu hizi mbili kwa kila goli watakalofunga. Tuwakilisheni vyema. Nawatakia kheri,” ameandika.

Simba SC inayoshiriki Klabu Bingwa Afrika itaikaribisha Raja Casablanca ya Morocco huku Yanga SC inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika ikiikaribisha TP Mazembe ya DR Congo.