TARURA wakabidhiwa magari 54

0
182

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewaagiza watendaji wa kata na viongozi wa mikoa wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kutumia vitendea kazi wanavyokabidhiwa na serikali katika kuwafikia wananchi kwa urahisi, kuwasikiliza, kuwahudumia, kufuatilia miradi ya maendeleo na siyo kutumia kwa manufaa binafsi.

Dkt. Mpango ametoa agizo hilo mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi magari 54 kwa TARURA pamoja na pikipiki 916 kwa watendaji kata, zilizotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Amewaagiza watendaji wa kata kutambua na kushughulikia changamoto za wananchi kwa kuhakikisha vikao na wananchi katika ngazi ya vijiji na mitaa vinafanyika kama inavyopaswa.

Pia Dkt. Mpango amewataka Wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha shilingi laki moja inayopaswa kutolewa kwa Maafisa Watendaji wa Kata kama posho ya madaraka inatolewa kwa wakati na kupewa kipaumbele kabla hazijalipwa posho za vikao vingine vya halmashauri.