Watuhumiwa wa pasipoti bandia mbaroni.

0
232

Idara ya Uhamiaji mkoani Pwani imewakamata watu wawili raia kutoka nchi za Nigeria na Cameroon kwa tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuishi nchini bila kibali, kujihusisha na biashara ya utengenezaji wa fedha bandia na utengenezaji wa hati bandia za kusafiria.

Mkuu wa mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo Abubakar Kunenge amesema, watuhumiwa hao wamekamatwa katika eneo la Mapinga wilayani Bagamoyo baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema.

Amesema baada ya watuhumiwa hao kukamatwa na kupekuliwa katika nyumba walimokuwa wakiishi wamekutwa na pasi za kusafiria ambazo zimeisha muda wake tangu mwaka 2020 na pia wamekutwa na karatasi za kutengenezea fedha bandia pamoja na pasi bandia za kusafiria 30.

Kunenge amesema watuhumiwa hao wote wawili hawana hadhi za kiuhamiaji, hivyo watafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika.