Panya Road 6 wakamatwa Dar

0
151

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watu sita wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu maarufu Panya Road.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema watu hao wamekamatwa wakati wa operesheni maalum inayoendelea katika maeneo ya Bunju A na Bunju B.

Akizungumza usiku wa kuamkia hii leo katika kituo cha polisi cha Mabwepande mara baada ya kufanya operesheni ya kushtukiza katika maeneo hayo, Kamanda Muliro amesema miongoni mwa watuhumiwa hao sita wamekamatwa katika maeneo ya Mapinga, Bagamoyo mpakani.

Amesema pamoja na kuwakamata watuhumiwa hao sita wanaodaiwa kufanya vitendo vya uhalifu, pia wamekamata baadhi ya vitu walivyoiba ikiwa ni pamoja na simu.

Kamanda Muliro amesisitiza kuwa Dar es Salaam ni shwari na kwamba polisi hawatamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuvunja amani na utulivu.