Pelé na historia ya alivyofikia kutumia jina hilo

0
601
(FILES) In this file photo taken on June 13, 1961 Brazilian striker Pelé, wearing his Santos jersey, smiles before playing a friendly soccer match with his club against the French club of "Racing", in Colombes, in the suburbs of Paris. - Brazilian football icon Pele, widely regarded as the greatest player of all time and a three-time World Cup winner who masterminded the 'beautiful game', died on December 29, 2022 at the age of 82, after battling kidney problems and colon cancer. (Photo by AFP)

Mashabiki na wasio mashabiki wa mpira, wengi wanamfahamu Pelé ambaye jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento, raia wa Brazil aliyebadili tafsiri na kufanya watu kuupenda mpira wa miguu.

Swali moja ambalo watu wengi wanajiuliza ni kuwa jina hili ‘Pelé’ lilitoka wapi?

Kwanza ifahamike kuwa Brazil wanapenda sana ‘nick names’ ndio sababu wachezaji wengi hata wanaofamika sasa duniani, wanafamika kwa majina ambayo si majina yao halisi akiwemo Ronaldinho Gaúcho, ambaye jina lake ni Ronaldo de Assis Moreira na Kaka anayetwa Ricardo Izecson dos Santos Leite.

Turudi kwa Pelé. Binafsi katika kitabu cha maisha yake anaeleza kuwa hakuwa analipenda jina hilo, na amewahi kugombana na watoto wenzake waliokuwa wakimuita jina hilo kama kumtania.

Katika maelezo yake, anasema kuwa golikipa wa timu ambayo baba yake alikuwa anaichezea alifahamika kwa jina la utani la Bile. Jina hili (Bile) alipewa ikiwa ni neno la kwanza alilosema alipoanza kuongea akiwa na umri wa zaidi ya miaka miwili, baada ya kufanyiwa shughuli ya kitamaduni kufuatia wazazi wake kuwa na hofu kwa kuchelewa kuongea.

Wakati Pelé alipokuwa akienda uwanjani kutazama timu ya baba yake ikicheza, alianza kumtania golikipa huyo kwa kumwita ‘Pile’ badala ya ‘Bile’ lakini kutokana na lafudhi yake yenye asili ya Kusini Mashariki mwa Brazil, watoto wenzake katika mji wa Bauru uliopo São Paulo walimsikia kama anataja jina ‘Pelé.’

Kuanzia hapo walianza kumtania, na kadiri alivyochukia ndivyo walivyozidisha utani huo. Pelé alipobaini hilo, aliamua kulikubali jina hilo ili kupunguza kutaniwa, na ndilo likawa jina linalomtambulisha duniani.

Itambulike kuwa, jina hilo halikuwa jina pekee la utani alilokuwa akiitwa na makundi mbalimbali ya watu, wengine walimwita Dico, wengine walimwita Gasolina.

Jambo jingine ambalo pengine watu hawalifahamu ni kuwa jina ‘Edson’ ambalo ni jina la kwanza la Pelé, alipewa na baba yake kama sehemu ya kumsherekea Thoman Edison aliyegundua ‘bulb’ ya umeme kwani wakati Pelé anazaliwa ndio umeme ulikuwa umefika kwenye eneo lao.