Waziri Ummy asisitiza uadilifu katika utoaji haki juu ya upimaji vinasaba

0
176

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa wito kwa watumishi wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa waadilifu na utendaji wa haki katika kuwahudumia wananchi wanaofika katika mamlaka hiyo hususan wanakuja kupata huduma za kupima vinasaba.

Waziri Ummy amesema hayo, wakati alipofanya ziara ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuongea na Watumishi katika ofisi hizo zilizopo Jijini Dodoma.

Amesema, “Kazi yenu hii inauhusiano wa karibu na mambo ya kutenda haki, na mimi kwasababu ni mwanamke, kwahiyo katika swala la kuchunguza uhalali wa baba wa mtoto ni yupi napenda sana tuwe waadilifu ili kutenda haki ya kweli bila kuonea yoyote.”

Sambamba na hilo, Waziri Ummy ameelekeza Taasisi zote za umma na binafsi kutenga vyumba na mabafu kwaajili ya watumishi wao kufanya mazoezi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupambana dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Nae, Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amesema, kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kutasaidia kusogeza huduma za kutosha kwa wananchi kutoka maeneo mbalimbali hasa katika mikoa ya mbali iliyokuwa ikipata huduma hizi Jijini Dar es Salaam.