Zanzibar kuendeleza ushirikiano na IAEA

0
540

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, -Simai Mohamed Said amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA)
ili kukuza na kuimarisha teknolojia ya utumiaji wa mionzi.

Naibu Waziri Simai ametoa kauli hiyo jijini Arusha wakati wa mkutano wa pamoja na ujumbe wa IAEA Kanda ya Afrika.

Ameongeza kuwa Zanzibar bado changa katika utumiaji wa teknolojia ya mionzi, hivyo ushirikiano huo utaisaidia kuimarisha utumiaji wa teknolojia hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) Kanda ya Afrika Profesa Shaukati Abdulrazak amesema kuwa lengo la shirika hilo ni kutumia teknolojia ya mionzi katika uzalishaji wa vyakula, kuondoa wadudu waharibifu wa mazao na kupambana na maradhi ya saratani.

Profesa Abdulrazak amesisitiza kuwa IAEA ipo tayari kuwajengea uwezo Wakazi wa Zanzibar ili waweze kutumia teknolojia ya mionzi kwa lengo la kujiletea maendeleo zaidi.

Amesema kuwa shirika hilo pia litahakikisha Zanzibar inapata kifaa maalumu kwa ajili kupimia maradhi ya saratani.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) Profesa Lazaro Busagala amesema kuwa kazi ya kwanza ya majaribio ya shirika hilo kwa Zanzibar ni kuhakikisha hakuna kabisa wadudu aina ya Mbung’o, jaribio ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Ameongeza kuwa ushirikiano ndio jambo linalohitajika hivi sasa ili kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo katika utumiaji wa Teknolojia ya mionzi.