Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amesema serikali imetenga shilingi bilioni 16.5 kufanya ukarabati wa hospitali 19 katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Dkt. Dugange ametoa kauli hiyo leo Bungeni mkoani Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti Maalum, Esther Midimi aliyetaka kujua Je, ni lini serikali itajenga hospitali ya wilaya katika halmashauri ya wilaya ya Meatu kwa kuwa hospitali iliyopo ina hadhi ya kituo cha afya na haikidhi mahitaji.
Dkt. Dugange amesema hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Meatu ni miongoni mwa hospitali kongwe 50, ilianza kutoa huduma kwa ngazi ya kituo cha Afya ambapo mwaka 1989 ilipandishwa hadhi na kuwa hospitali.
Aidha, Dkt. Dugange amesema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga fedha za ukarabati wa hospitali 31 zilizobakia ikiwemo hospitali ya wilaya ya Meatu.