Nigeria yavuliwa umiliki wa Jollof

0
316

Baada ya mvutano wa miaka mingi kuhusu nani ni mmiliki wa asili wa mapishi ya wali wa Pilau la Afrika Magharibi maarufu kama ‘Jollof’ kati ya nchi za Nigeria, Ghana, Senegal na Cameroon, hatimaye Senegal imetangazwa na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) kuwa mfalme wa chakula hicho.

Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO umesema baada ya kushindanishwa kwa chakula cha Jollof cha nchi hizo nne, Senegal iliibuka kidedea kutangazwa kuwa mwanzilishi wa kweli wa chakula hicho.

UNESCO imeiweka Jollof kwenye orodha ya urithi wa kitamaduni, ikiwa ni ishara ya namna Wasenegal wameshawishi aina mbalimbali za upishi wa wali wa Jollof.

Jollof inaaminika kuwa asili yake ni jamii ya wavuvi katika kisiwa cha Saint-Louis nchini Senegal na inatayarishwa kwa kuchanganya mchele, samaki, nyanya, mboga mboga na viungo vingine.

“Chakula hicho kwa kawaida hutengenezwa kwa mnofu wa samaki, mchele uliovunjika, samaki waliokaushwa, moluska na mboga za msimu kama vile vitunguu, giligilani, vitunguu saumu, pilipili hoho, nyanya, karoti, biringanya, kabichi nyeupe, mihogo, viazi vitamu, bamia na jani la ‘bay’,” UNESCO imesema.

Kulingana na utafiti uliofanywa na taasisi ya Conversation Africa, chimbuko la wali wa Jollof lilianzia wakati wa utawala wa kikoloni Afrika Magharibi kati ya mwaka 1860 na 1940.

Awali, chakula hicho kilijizolea umaarufu kwenye nchi nyingi kama chakula cha Wanigeria.