Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote (UHC) ambao ulikuwa uwasilishwe bungeni leo Alhamisi 9, 2023 jijini Dodoma umekwama kwa mara nyingine, kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya mambo katika utekelezaji wa muswada huo.
Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameliambia Bunge kuwa muswada huo ambao ulikuwa uanze kujadiliwa bungeni leo na kesho, umerudishwa kwenye kamati kwa ajili ya kujadiliwa zaidi na kisha utapelekwa Bungeni katika mikutano inayofuta.
Dkt. Tulia amesema muswada wa Bima ya Afya kwa Wote umesogezwa mbele mpaka wakati mwingine ambapo kwa sasa majadiliano yanaendelea na hasa eneo la bajeti na utekelezaji wa muswada huo.
Hii ni mara ya pili muswada huo kukwama tangu usomwe kwa mara ya kwanza bungeni katika mkutano wa nane wa Bunge na kupelekwa katika kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuchambuliwa.