Watoto 20 mikoni Mwa Polisi Geita

0
185

Jeshi la polisi mkoani Geita limefanya operesheni maalum na kuwakamata watoto 20 katika maeneo mbalimbali mkoani humo kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Geita, Safia Jongo amesema watoto hao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya
unyang’anyi na uporaji wa simu na vitu vingine vidogo vidogo.

Amesema wengi wa watoto hao wamekamatwa
katika maeneo yanayozunguka nyumba za starehe na kwamba wanadaiwa kufanya vitendo hivyo kwa watu pindi wanapotoka katika maeneo hayo.

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi wa TBC mkoani Geita Kamanda Jongo amesema, wamefanya operesheni hiyo maalum ya kuwakamata watoto hao kufuatia kukithiri kwa wimbi la watoto kusafiri kutoka maeneo mbalimbali kwenda miji mikubwa na kufanya vitendo vya uhalifu.

Kuhusu watoto sita waliokamatwa mkoani humo wakiwa wanasafiri kutoka Bukoba mkoani Kagera kwenda Mwanza kwa kujificha chini ya uvungu wa basi, Kamanda Jongo amesema watoto hao wapo katika uangalizi maalum.

Amesema kinachofanyika hivi sasa ni kuwasiliana na ndugu zao wa maeneo wanayotoka ili kujua ukweli kama wazazi wao wapo au la.