Abdullah asifu maboresho sekta ya afya Tanga

0
120

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah ameeleza kufurahishwa na maboresho ya sekta ya afya mkoani Tanga hasa katika hospitali ya Rufaa ya Bombo ambapo huduma ya kusafisha damu inatolewa.
 
Makamu wa Pili wa Rais ambaye ni Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga yupo mkoani humo ambapo leo ameshiriki maandamano ya wanachama wa chama hicho na kisha kutembelea miradi ya kimkakati iliyotekelezwa kwenye Ilani ya CCM ikiwamo hospitali ya Bombo na Bandari ya Tanga akifuatana na viongozi mbalimbali.
 


Akiwa hospitalini hapo ametembelea chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, wodi ya watoto njiti, chumba cha mashine ya uchunguzi na wagonjwa wa figo wanaofanya huduma ya kusafisha damu.
 
“Nimeshangazwa na maboresho ya huduma za afya katika hospitali hii, sikuamini nilipoambiwa tunakwenda kuangalia wagonjwa wanaofanyiwa dialysis, nilijua tunakwenda kuangalia orodha ya wagonjwa wanaokwenda Muhimbili kufanyiwa huduma hiyo, haya ni maboresho makubwa mno kwa sekta ya afya,” amesema Abdullah
 
Amewataka wakazi wa mkoa wa Tanga kuunga mkono muswada wa bima ya afya kwa wote ili kupata unafuu wa gharama za matibabu na kuwa na uhakika wa matibabu.