Wakazi elfu 6 kunufaika na mradi wa maji Tukuyu

0
176

Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Jaffar Haniu amefanya ziara katika chanzo cha maji Mbaka – Ikama kilichopo katika kata ya Itagata barabara ya Katumba -Mwakaleli.

Akiwa katika chanzo hicho Haniu ameuagiza uongozi wa Mamlaka ya Maji Tukuyu Mjini (TUWASA) kuharakisha upanuzi wa chanzo hicho ili kutoa fursa ya kuhudumia zaidi ya wakazi elfu sita wanaishio Tukuyu Mjini.

“Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi sana kwa ajili ya upanuzi wa chanzo hiki, zaidi ya shilingi Bilioni 3.4 zimetolewa hivyo niwaagize mfanye kazi kwa bidii na weledi ili tuwasogezee hii huduma muhimu katika maeneo yao.” ameagiza Haniu

Mradi huo ulionza kusanifiwa mwaka 2021 unatarajiwa kuzalisha zaidi ya lita elfu 45 za maji kwa siku huku mahitaji yakiwa ni lita elfu 22 kwa siku ifikapo mwaka 2042 na hivyo kutoa ziada ya maji katika mji wa Tukuyu.

Unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu ambapo shughuli za ujenzi zimefikia asilimia 80 zikihusisha ulazaji wa bomba kuu la mserereko.

Akiwa katika eneo la ujenzi wa tenki la maji katika soko la ndizi Msasani, Haniu amemuagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kwa wakati kazi hiyo na kuleta tija na maendeleo kwa wananchi.