Butiku : Uzalendo unaanza kwenye familia

0
238

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema kuna umuhimu wa kuanzishwa kwa Jukwaa la Uzalendo Kitaifa.

Butiku amesema hayo mkoani Dar es Salaam alipotembelea ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), ambapo akiwa ofisini hapo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha.

Butiku amesema kuanzishwa kwa Jukwaa hilo la Uzalendo Kitaifa kutasaidia familia kutengeneza kitovu cha uzalendo na hasa malezi ya awali katika jamii.

Amesema pia litalifanya Taifa kuwa lenye utu, haki sawa na Taifa lenye kuzungumza lugha moja.

“Makongamano mengi hayaji na njia za utatuzi wa matatizo ya jamii, tuanzishe Jukwaa la Uzalendo hasa kwenye familia maana misingi ya haki za binadamu huanzia hapo, watu na watoto wenye tabia mbaya na njema huanzia hapo, maisha ya utu yamepotea kwa kiasi kikubwa nchini.” amesema Butiku

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha amesema Jukwaa hilo litazalisha vijana wenye kuthamini na kujali Taifa lao.

“Chukulia dereva pikipiki (Bodaboda) anavuka tu barabarani wakati taa za barabarani hazijamruhusu, mtu huyo asipo jengwa kichwani mwake kutokuvunja sheria atachulia ni kawaida na itapelekea atavunja sheria zingine ambazo si za barabarani, ni muhimu wakapata elimu kupitia jukwaa la Uzalendo.” amesema Dkt. Rioba