NASAHA ZA ASKOFU MAFUJA BAADA YA KUSIMIKWA

0
166

Askofu wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani ambaye amesimikwa leo amewasihi wakristo kwa ujumla na waumini wa kanisa la AICT kutoa malezi bora kwa watoto wao ikiwemo kuwapa fursa ya kupata elimu pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudumisha amani.

Akikumbusha mambo muhimu ya kuzingatia ili kudumisha amani ya taifa la Tanzania amewasihi wachungaji kushirikiana katika kuhubiri na kufundisha kwa usahihi neno la Mungu na kusema kuwa ndio injili pekee yenye nguvu ya kumbadilisha mtu na kumfanya kuwa raia mwema ili kuisaidia serikali inayopambana na kutokomeza maovu.

Askofu Mafuja ameahidi kutumia cheo kipya alichosimikwa leo kujenga ustawi wa Taifa la Tanzania huku akiwakumbusha wazazi na walezi kuona umuhimu wa elimu kwa watoto kwa kuwapeleka watoto shule huku wakichukia na kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto vinavyotendeka katika jamii.

Aidha, amewasihi waumini wa kanisa hilo kuendelea kumwombea ili atekeleze majukumu sawa na kiapo chake na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyolea Taifa la Tanzania na kuchochea maendeleo.

Askofu Philipo Mafuja awali alikuwa Askofu wa Dayosisi ya Mwanza na hii leo amesimikwa kuwa Askofu wa Tatu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Pwani, katika Kanisa la AICT lililopo Magomeni, Dar es Salaam.