DKT. MPANGO: TUSIWE CHANZO CHA KUKUZA MIGOGORO KATIKA KANISA

0
174

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewakumbusha waumini wa dini ya kikristo kudumisha ushirikiano baina yao na viongozi wa kanisa kama sehemu ya kutokomeza migogoro kanisani.

Dkt. Mpango ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika ibada maalumu ya kumsimika Askofu wa Dayosisi ya Pwani, Philipo Mafuja katika kanisa la AICT lililopo Magomeni, Dar es Salaam.

Amewakumbusha viongozi wa dini kutojilimbikizia mali na kuwa na uchu wa madaraka isivyo sawa na wito wao kama watumishi wa kanisa bali watumikie nafasi walizonazo kwa uaminifu na unyenyekevu huku akipongeza uongozi wa kanisa hilo kwa kuwa na sifa njema ya kanisa la kikristo.

Sambamba na hayo amewasihi viongozi wa dini kuendelea kulea Taifa la Tanzania kimaadili huku wakikemea maovu na vitendo visivyoendana na mila na tamaduni za Tanzania.

Kwa upande mwingine Dkt. Mpango ameshukuru kanisa la AICT nchini kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali ya Tanzania katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya huduma za kijamii mijini na vijijini.

Aidha, Dkt. Mpango amechangia kiasi cha shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa kanisa la AICT lililopo Magomeni na kusema kuwa  Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano baina yake na madhehebu yote ya dini nchini huku akitolea majibu ya maombi ya kanisa papo hapo yaliyowasilishwa wakati wa kusoma hotuba akielekeza wizara na mamlaka husika kushughulikia maombi yao yanayohusu utatuzi wa mgogoro wa viwanja na ujenzi wa kanisa.